Kuhusu Shirika la Kukodisha Nyumba la Stockholm

Shirika la Kukodisha Nyumba la Stockholm (Bostadsförmedlingen) ni kampuni ya manispaa ambayo inapeana makazi kutoka kwa wamiliki wa mali ya manispaa na ya kibinafsi katika eneo lote la Stockholm. Tunakodisha makao takriban 20,000 kila mwaka, lakini hatujengi au kumiliki makazi yoyote.

Shirika la Kukodisha Nyumba la Stockholm – jinsi linavyofanya kazi

Shirika la Kukodisha Nyumba la Stockholm hukuwezesha kutuma maombi ya kupata makazi kwenye nyumba za kukodisha zisizo na wapangaji katika eneo la Stockholm. Makazi hutengwa kupitia mfumo wa foleni kulingana na wakati ombi lako linapokelewa kwenye foleni ya maombi. Ili kutuma maombi ya kupata makazi, lazima ujiandikishe kwenye foleni ya kukodisha nyumba.

Je, ni nani anaweza kujiandikisha kwa foleni ya kukodisha nyumba?

Mtu yeyote aliye na umri wa miaka 18 na aliye na  nambari ya utambulisho wa kibinafsi ya Uswidi (personnummer) au nambari ya uratibu (samordningsnummer) anaweza kujiandikisha kwenye foleni ya kukodisha nyumba. Haijalishi unaishi wapi au ikiwa tayari una makazi. Mara tu baada ya kujiandikisha, utawekwa kwenye foleni ya kukodisha nyumba. Kisha unaweza kuanza kutuma maombi ya kukodi nyumba na kujiandisha kwa ajili ya kupata nyumba kulingana na mapendeleo yako maalum. Kuwa katika foleni ya kupata nyumba kunagharimu Krona (SEK) 200 za Uswidi kwa mwaka.

Aina tofauti za makazi

Shirika la Kukodisha Nyumba la Stockholm lina aina tofauti za nyumba. Nyingi za nyumba hizi zinaweza kukodishwa kwa yeyote aliye kwenye foleni ya kukodisha nyumba, lakini nyumba fulani zimehifahiwa kwa vikundi maalum.

  • Nyumba za wanafunzi: Kwa wale wanaosoma katika chuo kikuu au chuo cha ufundi.
  • Nyumba za vijana: Kwa walio na umri wa miaka kati ya 18 na 25.
  • Nyumba za wazee: Kwa walio na umri wa miaka 55 au zaidi.
  • Mkataba wa muda mfupi: Makubaliano ya kipindi kifupi cha malazi. Ikiwa umepewa mkataba wa muda mfupi, utazingatia wakati wako wa kusubiri kwenye foleni.

Kutuma maombi ya kukodisha nyumba

Lazima wewe binafsi uombe nafasi za makazi zilizotangazwa kwenye tovuti yetu. Kila tangazo lina habari za kina kuhusu makazi hayo pamoja na masharti ya kupangisha ya mwenye nyumba. Ukishaingia kwenye akaunti, unaweza kuonyesha kuvutiwa kwako na nyumba fulani kupitia kwa tangazo hilo moja kwa moja. Jinsi unavyotafuta kwa bidii, ndivyo unakavyokuwa na nafasi kubwa ya kupata makazi.

Je,inachukua muda gani kupata makazi?

Muda utakaosubiri kwenye foleni hutegemea mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na mahali unapotaka kuishi na kiwango cha kodi unachoweza kumudu. Muda wa wastani wa kusubiri kwenye foleni ni miaka tisa, lakini unaweza kuwa mfupi au zaidi. Mara nyingi, muda kwenye foleni huwa mrefu zaidi katika makazi yaliyoko mjini Stockholm au maeneo ya jirani ikilinganishwa na maeneo yaliyo mbali na mji.
 
Kuwekwa nafasi ya kwanza kwenye foleni: Ikiwa una sababu kubwa za kiafya au kijamii, unaweza kuomba nafasi ya kwanza kwenye foleni. Hata hivyo, ni idadi ndogo tu ya watu ambao wanatimiza masharti ya kupewa nafasi ya kuzingatiwa kwanza.

Jinsi ya kupata makazi

Hapa,  unaweza kuona hatua kwa hatua jinsi ya kupata makazi kupitia kwetu. Ili uweze kutafuta nyumba, ni lazima kwanza uwe umesajiliwa kama mtu anayetafuta nyumba. Unapaswa kujiandikisha kwenye tovuti yetu, na utahitaji kutumia kitambulisho cha kielektroniki (e-ID). Iwapo huwezi kutumia kitambulisho cha kielektroniki, unaweza kuwasiliana na huduma yetu kwa wateja badala yake, na watakusaidia kujiandikisha.

1. Ombi la kupata nyumba

Unaweza kutafuta matangazo katika Lediga bostäder (Vacant dwellings) kwenye tovuti yetu. Hapa, unaweza kuchuja utafutaji wako kulingana na vigezo mbalimbali ili uweze kuona kwa urahisi nyumba tu ambazo zinakufaa. Ili kuandikisha nia yako, unahitaji kuingia kwenye akaunti. Unaweza kufuata maendeleo ya ombi lako kwenye Mina sidor (My Pages). Kwa kawaida, nyumba hutangazwa kwa siku 3-7.

2. Nenda kwenye kutazama na uthibitishe nia yako

Ikiwa wewe ni mmoja wa watuma maombi ya kupangisha nyumba walio na muda mrefu zaidi kwenye foleni, utapokea mwaliko wa kutazama nyumba mara tu kipindi cha maombi kitakapomalizika. Wamiliki wengine wa nyumba huhitaji mtu ambaye anapewa nyumba awe aliiona kabla ya kutia sahihi kwenye makubaliano. Kwa hivyo, ni muhimu kusoma sheria na masharti yanayotumika katika makao unayovutiwa nayo.
 
Baada ya kutazama nyumba, unahitaji kuthibitisha ikiwa bado unavutiwa na makao hayo. Njia rahisi ya kufanya hivyo ni kupitia Mina sidor (My Pages), ambapo unaweza kujibu ndio au hapana.
 
Wakati mwingine unaweza kupewa zaidi ya chaguo moja, haswa kukiwa na nyumba na makazi mapya. Ikiwa ni hivyo, lazima uthibitishe katika mpangilio zile nyumba unazozipa kipaumbele. Tarehe ya mwisho ya kujibu itaonyeshwa kwenye mwaliko wa kutazama.

Kumbuka: Wamiliki wengine wa nyumba hawatoi nafasi ya kutazama nyumba. Basi unaweza kuamua kama unataka makazi hayo kwa kutegemea habari iliyo kwenye tangazo hilo. 

3. Kupeanwa kwa nyumba na cheti

Ikiwa unatimiza masharti ya mmiliki wa nyumba na umekuwa kwenye foleni kwa muda mrefu zaidi, utapewa nafasi ya kupata na kukodi nyumba pamoja na maelekezo ya hatua inayofuata. Kisha utahitaji kutuma nyaraka za kuthibitisha maelezo yako. Kwa hivyo, unapaswa kuhakikisha kuwa maelezo yako ni ya hivi karibuni katika Mina sidor (My pages) (maelezo ya mawasiliano, mapato, mwajiri, nk).

4. Kutia sahihi kwenye makubaliano

Mara tu baada ya kutuma cheti chako na kimeidhinishwa nasi, tutatuma maelezo yako kwa mmiliki wa nyumba na kukupendekeza kama mpangaji. Iwapo mmiliki wa nyumba atakukubali, unaweza kutia saini kwenye makubaliano.

Mara baada ya kutia sahihi kwenye makubaliano ya ukodishaji wakati wako kwenye foleni utarekebishwa, lakini utabaki kwenye foleni kiotomatiki mradi tu utalipa ada ya kila mwaka. Katika hali nyingine, unaweza kuendelea kuwa kwenye foleni. Hii inatumika ikiwa makubaliano yako yanahusiana na aina yoyote kati ya makao yafuatayo:

  • Nyumba za wazee
  • Nyumba za wanafunzi
  • Nyumba za vijana
  • Mkataba wa muda mfupi

Mina sidor (My Pages)

Kwenye Mina sidor (My pages), unaweza kuona nyumba ambazo umependezwa nazo. Unaweza pia kupata taarifa kuhusu muda wako katika foleni na ada ya mwaka hapa, na unaweza kusasisha maelezo yako ya kibinafsi. Unapaswa kuingia katika akaunti yako ili uweze  kufikia Mina sidor (My Pages).

Kuingia katika akaunti

Njia rahisi na salama zaidi ya kuingia katika akaunti ni kupitia kitambulisho cha kielektroniki (BankID au Freja eID+). Ikiwa huna kitambulisho cha kielektroniki, unaweza kufungua akaunti kwa kutumia anwani ya barua pepe na nenosiri.

Maelezo ya mawasiliano

Huduma kwa wateja
Namba ya simu: 08-785 88 30
Barua pepe: kundservice@bostad.stockholm.se

Sanduku la posta
Bostadsförmedlingen i Stockholm AB
Box 7026
121 07 Stockholm-Globen